Misingi bora ya jamii ni chanzo cha haki na usawa
1 April 2021, 11:24 am
Na; Mindi Joseph.
Kituo cha sheria na haki za Binadamu kimemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassani kutengeneza misingi itakayohakikisha jamii inaishi kwa kufuata sheria haki na kuzingatia usawa wa kijinsia.
Akizungumza na Taswira ya habari hii leo Bw.Joramu Bwire kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu, amesema kama jamii itaishi katika misingi ya kufuata sheria itasaidia kuendelea kuwepo kwa haki na usawa.
Ameongeza kuwa kituo cha sheria na haki za Binadamu kipo mstari wa mbele katika kuhakikisha haki kwa jamii inaendelea kuwepo kwani mpaka sasa kimefanikiwa kuunda vilabu 177 katika shule za msingi ,Sekondari na Vyuo vikuu katika kutoa elimu kuhusu sheria na haki za binadamu.
Katika hatua nyingine amesema Kituo cha sheria na haki za Binadamu kitaendelea kumuenzi hayati Dkt.John Pombe Magufuli kwa kufanya nao kazi pamoja na kulinda haki za binadamu.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilianzishwa Mwaka 1995 kwa lengo la kuwajengea uwezo Watanzania juu ya sheria na haki zao ili kuendeleza, kuimarisha na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini.