Rais Magufuli aliutambua mchango wa wanawake katika uongozi
24 March 2021, 12:06 pm
Na; Mariam Matundu.
Viongozi wanawake jijini Dodoma wamesema watamkumbuka daima hayati Dkt.John Magufuli kwa kuwa aliwaamini wanawake na kuwapa nafasi mbali mbali za uongozi katika kipindi cha uongozi wake.
Akizungumza na taswira ya habari mmoja wa madiwani wanawake Kata ya Kilimani jijini Dodoma Neema Mwaluko, amesema hayati Dkt.Magufuli ni rais wa kwanza Tanzania kumteua mwanamke kuwa makamu wa rais jambo ambalo limehamasisha wanawake wengi kujiamini.
Aidha amesema wanawake viongozi katika sekta mbalimbali hawana budi kuyaenzi ya hayati Dkt.Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu ili kuendelea kuiambia Dunia kuwa wanawake wanauwezo wa kufanya jambo lolote sawasawa na wanaume .
Hayati Dkt.Magufuli katika kipindi cha uhai na uongozi wake aliwateua wanawake zaidi ya 5 katika nafasi za uwaziri na ambao wamedumu katika nafasi hizo bila kubadilishwa tangu kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya awamu ya kwanza hadi sasa ni pamoja na waziri wa elimu ,sayansi na teknolojia prof . Joyce Ndalichako na waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh.Jenista Muhagama.