Hatimae Samia Suluhu aapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
19 March 2021, 8:24 am
Na, Mariam Kasawa.
Aliyekua makamu wa Rais wa awamu ya tano Mh. Samia Suluhu Hassani hatimaye ameapishwa leo kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mara ya kwanza leo machi 19, 2021 Tanzania imeandika historia ya kupata rais mwanamke ambae amechukua nafasi ya hayati Dkt John Pombe Magufuli ambae amefariki Dunia machi 17 kwa tatizo la moyo.
Hafla ya kuapishwa kwake imefanyika ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.
Akizungumza baada ya kuapishwa kwake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassani amewashukuru viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kwa kuwa na mshikamono hususani kipindi hiki kigumu cha msiba .
Aidha amewaahidi wananchi kuwa hakuna kitu kitakacho haribika na kuwataka kusonga mbele, na kwamba huu ni wakati wa kufarijiana, kufutana machozi pamoja na kuomboleza ili kumuenzi hayati Dkt. John Pombe magufuli.
Rais Mh. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku 21 za maombolezo ambapo Bendera zitapepea nusu mlingoti.