Wananchi Muungano walalamika kufanyishwa usafi katika zahanati
15 January 2025, 4:14 pm
Licha ya ukubwa wa kijiji cha Muungano lakini zahanati hiyo ina watumishi wawili ingawa kwasasa imebaki na mtumishi mmoja kutokana na mtumishi mwingine kuwa likizo.
Na Victor Chigwada .
Wananchi kijiji cha Muungano wamelalamikia kufanyishwa usafi katika zahanati inayopatikana kijijini hapo tofauti na huduma ya msingi iliyowapeleka hapo.
Wakizungumza na Taswira ya Habari baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wameshangazwa na hali hiyo ambapo akina mama wajawazito na wagonjwa wamekuwa wakifanyishwa usafi hasa kufagia eneo la zahanati hiyo kabla ya kupata Huduma ya Mama na Mtoto.
Aidha wameiomba Serikali kuongeza watumishi kwa ajili ya usafi.
Florensia Msimbili ni muhudumu wa afya ngazi ya jamii katika zahanati hiyo amekiri uhaba wa watumishi hivyo wagonjwa hulazimika kufanya zoezi la usafi wa mazingira.
Amesema hali hiyo inapelekea wananchi wanaowahi kufika zahanati hiyo kwa ajili ya kupata huduma za afya kusaidia zoezi la usafi ili kuharakikisha shughuli hiyo ili waweze kupata huduma.
Msimbili ameongeza kuwa wanampango wa kuongeaa na Serikali ya kijiji ili kuona namna ya kuajiri mtu ambaye atahusika na zoezi la usafi .