Marie Stopes yazindua kampeni ya ‘kwa kila hatua ya mwanamke’
27 October 2024, 6:13 pm
Kwa kutambua changamoto katika hatua ya ukuaji wa mwanamke na uhitaji wa huduma za afya, shirika la Marie Stopes Tanzania limezindua kampeni itakayomwezesha mwanamke kuanzia umri wa miaka 16 hadi 50 kupata huduma stahili za afya.
Na Hilali A. Ruhundwa, Wazalendo Media
Serikali imeahidi kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi zinazojihusisha na utoaji wa huduma za afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya. Hayo yamebainishwa na mwakilishi wa Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Living Nyaki ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya mwaka mmoja ya Kwa Kila Hatua ya Mwanamke, kampeni iliyozinduliwa Oktoba 25, 2024 jijini Dar es Salaam.
Akielezea huduma zitolewazo na hospitali za Marie Stopes Tanzania, Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo Bw. Patrick Nemo amesema kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kutoa huduma za afya hasa afya ya uzazi na kwamba kampeni hii ni sehemu ya kuwahudumia wanawake baada ya kubaini kuwa wanapitia changamoto nyingi katika hatua zote za ukuaji.
Kwa upande wake Mratibu wa kampeni hiyo Dkt. Mashingo Lerise amesema kuwa kwa mwaka jana walitoa huduma kwa wanawake zaidi ya 98,000 na sasa wanatajia kuwafikiwa wanawake zaidi ya 100,000 ambao kila mmoja atawafikia wanawake wengine 10 na kufikia zaidi ya wanawake milioni moja.
Lisa Chonya ni miongoni mwa mabinti wanaotegemea kunufaika na kampeni hiyo na hapa anaelezea jinsi atakavyofaidika.
Shirika la Marie Stopes Tanzania limekuwa likitoa huduma za afya nchini kwa miaka mingi kupitia vituo vyake vya afya vilivyopo mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuifikia jamii ya vijijini.