Serikali yatenga fedha kuimarisha usimamizi na uratibu wa lishe
19 April 2021, 12:48 pm
Na; Mariam Matundu
Serikali kupitia Halmashauri nchini imetenga shilingi elfu moja(1000) kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano ili kutekeleza afua mbalimbali za lishe ikiwemo kuanzisha kamati elekezi yenye lengo la kuimarisha usimamizi na uratibu wa suala la lishe.
Waziri mkuu Kassimu Majaliwa amezungumza wakati akizindua ajenda ya kitaifa ya kuwekeza katika afya na maendeleo kwa vijana balehe mwishoni mwa wiki ambapo moja ya nguzo katika ajenda hiyo ni kuimarisha hali ya lishe katika kundi hilo.
Aidha amewataka maafisa maendeleo ya jamii katika ngazi ya Kata na Vijiji kushirikishwa kikamilifu ili kwenda kutoa elimu katika jamii kuhusu masuala ya lishe bora.
Kwa upande wake waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt.Doroth Gwajima amesema asilimia 7.3% ya wanawake waliopo katika umri wa mika 15 hadi 49 wako katika uzito unaostahili hivyo ni muhimu kuwekeza katika suala la lishe kwa jamii.
Ajenda ya kitaifa ya kuwekeza katika afya na maendeleo kwa vijana balehe wenye umri wa miaka 10 hadi 19 ya mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025 imebebwa na nguzo tano za utekelezaji ambazo ni kuzuia na kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi, mimba na ndoa za utotoni , ukatili wa kimwili na kisaikolojia , kuboresha hali ya lishe , kuhakikisha watoto wa kike na wakiume wanabki shuleni pamoja na vijana balehe kutambua fursa za kiuchumi.