Dodoma FM

Wafanyabiashara Sabasaba walalamikia uwepo wa dampo katikati ya soko

10 December 2024, 4:50 pm

Maji yanayotiririka sokoni na kutuama, pamoja na harufu mbaya kutoka dampo hilo, vinaathiri mazingira ya biashara.Picha na Mariam Salum.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa soko la Sabasaba amesema soko hilo linahudumia zaidi ya wafanyabiashara 10,000, na kila siku zaidi ya watu 15,000 huingia na kutoka sokoni hapo, jambo linaloonesha ukubwa na umuhimu wa soko hili katika uchumi wa jiji la Dodoma.

Na Mariam Salum.
Wafanyabiashara wa soko la Saba Saba jijini Dodoma wanakabiliwa na changamoto ya miundombinu duni na uwepo wa dampo la taka katikati ya soko hilo, hali inayoathiri biashara zao.
Wakizungumza na Taswira ya Habari, wafanyabiashara hao wameeleza kuwa maji yanayotiririka sokoni na kutuama, pamoja na harufu mbaya kutoka dampo hilo, vinaathiri mazingira ya biashara na usalama wa bidhaa zao.
Aidha, Wafanyabiashara hao pia wamesema Barabara ya kuingilia sokoni hapo imekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara na wateja, hali inayozuia usafirishaji wa bidhaa na wateja kushindwa kufika kwa urahisi.

Picha ni muonekano wa mazingira katika soko la Sabasaba msimu huu wa mvua.Picha na Mariam Salum.

Mwenyekiti wa soko la Sabasaba, Athumani Abdallah, amethibitisha kuwa soko hilo lipo kwenye mpango wa kujengwa upya ili kukabiliana na changamoto za miundombinu na kuboresha huduma kwa wafanyabiashara na wateja.