Uongozi wa kijiji wakwamisha ujenzi wa shule ya sekondari Manungu
24 April 2023, 1:20 pm
Wananchi wamesema wao hawana tatizo bali wanataka viongozi wafikie muafaka kuwa shule hiyo ijengwe wapi.
NA Bernadetha Mwakilabi, Kongwa
Wananchi wa kijiji cha Manungu kilichopo kata ya Sejeli wilayani Kongwa wameulalamikia uongozi wa halmashauri ya kijiji hicho hususani mwenyekiti kwa kwa kuwagawa katika pande mbili za Chinyika A na Manungu A suala linalokwamisha maandalizi ya kupata eneo la kujenga shule ya sekondari ya Manungu .
Wananchi hao wameyasema hayo katika mkutano wa hadhara na Mkuu wa wilaya ya Kongwa ambapo wamesema kuwa wao hawana tatizo lolote kama viongozi wa kijiji wangekaa na kuafikiana shule ijengwe wapi na sio kuleta malumbano na wananchi.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Sejeli Mheshimiwa Chilingo Chimeledya amesema kuwa shule inatakiwa ijengwe eidha kitongoji cha Manungu A shule ya msingi au Chinyika A eneo ambalo wataalam wa halmashauri walifika na kuona linafaa kwa ujenzi japo wananchi hawakuliafiki.
Akitolea majibu mvutano huo Mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel amesema kuwa shule hiyo itajengwa katika eneo ambalo wataalam wameshauri ambalo ni Chinyika A karibu na tanki la maji la kijiji hicho hivyo atakaa na wazee na viongozi ili kuondoa tofauti hizo zinazokwamisha maendeleo.
Sambamba na hayo Mwema amesema kuwa Viongozi wa dini na wazee watumie nafasi zao vizuri kuunganisha wananchi kuondoa chuki zao na kuishi kwa umoja.