Wafugaji Bahi watakiwa kuheshimu miundombinu ya barabara
11 April 2023, 3:57 pm
Mifugo inapopitishwa kwenye barabara inaharibu miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa kwa serikali pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo husika.
Na Bernad Magawa.
Wito umetolewa kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo wilayani Bahi kulinda na kuheshimu miundombinu ya barabara kwani serikali inatumia fedha nyingi kurekebisha na kujenga miundombinu hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Bahi Stuwart Masima amekutana na makundi makubwa ya mifugo yakiswagwa barabarani wakati akikagua miundombinu hiyo wilayani Bahi, hali inayomlazimu kukemea vikali kuhusiana na uharibifu wa mifugo katika miundombinu ya barabara.
Amesema mifugo inapopitishwa kwenye barabara inaharibu miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa kwa serikali pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo husika kwani wanaitegemea miundombinu hiyo kwa maendeleo.
Masima amewataka wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo wilayani humo kufuata maelekezo ya serikali kuhusu matumizi ya mifugo kwenye barabara ambayo ni kuvuka na siyo kuswaga mifugo barabarani.