Serikali yapongezwa kwa kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurudi shule
30 November 2021, 12:56 pm
Na; Yussuph Hans.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepongeza hatua ya serikali kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurudi shuleni baada ya kujifungua.
Akitoa taarifa hiyo Jijini Dodoma Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Khamis Hamad amesema kuwa hatua hiyo ni ya kupongezwa kutokana na kuzingatia utoaji wa elimu bila ya ubaguzi Nchini.
Aidha amesema kuwa uamuzi huo pia ni hatua nzuri ya utekelezaji wa mkakati wa maendeleo wa kiuchumi na kijamii wa bara la afrika katika kujenga mtaji wa rasilimali watu kupitia uwekezaji wa elimu.
Taswira ya habari imezungumza na baadhi ya Wazazi na Wanafunzi katika jiji la dodoma kufahamu namna gani wanakuwa karibu kuzungumzia changamoto mbalimbali za kimasomo pamoja na Elimu ya afya ya Uzazi ambapo baadhi yao wamesema ni nadra kwa wazazi kuzungumzia suala hilo.
Pamoja na hayo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa mapendekezo mbalimbali ikiwepo Serikali kukaa pamoja na wadau wa elimu kuandaa na kupitia sera, sheria, mikakati na miongozo itakayosimamia utekelezaji wa azma hiyo na kuweka mazingira wezeshi kwa watoto wanaorejea shuleni ili kuto kuwepo kwa aina yoyote ya unyanyapaa.