Ukosefu wa mitaji na masoko ya kuuzia bidhaa ni changamoto kwa wajasiriamali wenye ulemavu
12 July 2021, 10:20 am
Na; Mariam Matundu.
Baadhi ya wajasiriamali wenye ulemavu Mkoani Dodoma wamesema ukosefu wa mitaji na masoko ya bidhaa zao ni moja ya sababu zinazopelekea wengi wao kushindwa kujiinua kiuchumi.
Mwita Marwa ambae ni mjasiriamali mwenye ulemavu amesema kutokana na changomoto hizo wengi wao wanakosa fursa mbalimbali ambazo zingeweza kupunguza viwango vya umasikini.
Amesema mara nyingi mazingira ya kazi kwao si rafiki na hata wanapotaka kutoa fursa kwa watu wengine wenye ulemavu kujifunza maeneo ya kazi hua ni madogo na hivyo ameiomba Serikali iwatafutie maeneo makubwa ya kazi.
Pamoja na hayo amesema suala la masoko ya bidhaa zao bado ni changamoto kubwa kwa kuwa watu wengi wenye ulemavu hawana uwezo wa kununua vifaa visaidizi mpaka wapate wafadhili.
Mmoja wa vijana waliofundishwa na Bw. Marwa, Michael Makalakala amesema bado kuna kundi kubwa la watu wenye ulemavu wanaopaswa kuwezeshwa ujuzi na mitaji ili waweze kujitafutia kipato.
Taswira ya habari imezungumza na mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Bw. Jabiri Shekimweli na amempongeza Bw. Mwita na kuahidi kumtembelea ili kuona namna ya kumsaidia.