Serikali yajipanga kuondoa mgao wa maji Nchini
29 April 2021, 1:15 pm
Na;Yussuph Hans
Serikali imesema inaendelea kujipanga kuhakikisha inaondoa adha ya mgao wa Maji kwa Wananchi katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.
Hayo yamebainishwa leo Bungeni na Naibu Waziri wa Maji Mh MarryPrisca Mahundi wakati akijibu swali la Mbunge wa Ndanda Mh Cecil Mwambe lilihoji nini mkakati wa serikali kuhakikishia Wananchi wa Ndanda wanapata Maji ya uhakika kuelekea Msimu wa kiangazi.
Mh Marryprisca amesema kuwa mpango mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tatizo la Maji linapungua Nchini, ambapo jitihada hizo zimesaidia kuwafikia wananchi wengi kutokana uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira RUWASA ili kushughulikia changamoto ya Maji.
Aidha naye Waziri wa Maji Mh Juma Aweso amesema kuwa wizara ya maji imepokea miradi 177 ambayo ni kichefuchefu ambapo kuna fedha zaidi Milioni Mia Tatu zimetengwa kwa ajili ya kukwamua miradi hiyo.
Kwa upande mwengine, Naibu Waziri wa Nishati Mh Stephen Byabato akijibu swali bungeni leo hii amesema kuwa katika kuhakikisha Mradi wa usambazaji umeme vijini REA unakamilika kwa wakati, serikali imeongeza usimamizi wa mradi, kupunguza wigo wa kazi za wakandarasi na kuhakikisha vifaa vyote vinavyohusika vipatikana Nchini.
Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini REA unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2022 ambapo sasa upo awamu ya tatu mzunguko wa pili ambapo ulianza Mwezi Machi 2021.