Klabu za mazingira zawajenga wanafunzi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
22 July 2024, 6:14 pm
Kuanzisha klabu ya mazingira ni rahisi, wanahitajika walimu ambao watakuwa walezi wa klabu pamoja na wanafunzi ambao wanapenda mazingira .
Na Mariam Kasawa.
Klabu za mazingira katika shule za msingi na sekondari zinatajwa kuwafundisha wanafunzi namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Elimu ya upandaji miti na bustani za mbogamboga zinazoanzishwa mashuleni zinawasaidia wanafunzi kufahamu umuhimu wa kutunza mazingira hata wanapokuwa nyumbani.
Klabu ya mazingira ni kikundi ambacho kinajishughulisha na uhifadhi wa mazingira ndani na nje ya shule. Wanachama wanashiriki kwenye klabu kwa hiari. Watapata elimu zaidi kuhusu mazingira na watafanya shughuli na miradi mingine kwa hiari.
Walimu wanasema klabu hizi zinasaidia sana kwani kupitia klabu hizi wanafunzi wamekuwa mabalozi wazuri wa mazingira kwa kuhamasishana wao kwa wao kupanda miti pamoja na kuanzisha bustani za mbogamboga.
Wadau wa mazingira wanasema utunzaji wa mazingira una faida kubwa hasa elimu hii inapotolewa kuanzia chini hususani kwa wanafunzi inasaidia kutengeneza mabalozi wa mazingira wa hapo baadaye.
Kwa upande wa wanafunzi wao wanasema klabu za mazingira zimeasaidia kufahamu njia nyingi za kutunza mazingira nyumbani na shuleni.