Msiwabebeshe mzigo watoto, fuateni mtaala wa elimu
23 February 2024, 5:38 pm
Mafunzo hayo kwa walimu wa elimu ya awali yana lengo la kuhalalisha elimu ya awali kuwa bora kwa mkoa mzima wa Dodoma.
Na Mariam Kasawa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.James Mdoe amewataka walimu wa madarasa ya awali kufundisha watoto kwa kufuata mtaala na siyo kuwafundisha masomo mengi yanayowalazimu kubeba mzigo wa begi la madaftari
Amesema walimu wanapaswa kuwafundisha watoto kwa kuwalea kwa sababu ndio kipindi ambacho wanakua ili waweze kuwa watoto wazuri walioandaliwa vizuri kwa ajili ya kujiunga na elimu ya shule ya msingi.
Prof. Mdoe amewataka washiriki wa mafunzo ya Walimu wa shule za Awali kuhakikisha wanawaandaa vyema watoto wote ili hapo baadae Taifa liweze kuwa na watu wengi walio elimika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Children in Crossfire, Craig Ferla amesema tafiti zilizofanya na Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOM) mwaka 2023, zinaonesha ya kwamba halmashauri 2 za wilaya ya Chamwino na Kongwa watoto katika darasa la awali wamefanya vizuri zaidi katika vipimo vyao Vya utayari wa shule, ukilinganisha na halmashauri zingine zenye mazingira yanayofanana.