Vijana wanufaika na Elimu ya usafi
15 April 2021, 12:23 pm
Na; Mindi Joseph
Jumla ya vijana elfu arobaini na nane Nchini wametajwa kunufaika na elimu ya usafi inayotolewa na Taasisi ya Raleigh Tanzania kupitia mradi wa vijana na mabadiliko chanya kitabia juu ya usafi.
Akizungumza na Taswira ya habari mratibu wa mradi huo Augustino Dickson amesema mradi unalenga kuleta mabadiliko chanya ya kitabia kwa vijana na unatekelezwa katika Mikoa 4 nchini ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Iringa na unahusisha zaidi vijana.
Kampeni hiyo imeanza mwezi Novemba mwaka jana na inatekelezwa kwa miezi 6 na vijana wengi wanaendelea kunufaika na elimu hiyo kwa kuwa pia inawainua kiuchumi.
Kwa upande wao baadhi ya vijana ambao ni wahamasishaji wa masuala ya usafi wamesema kuwa kampeni hii inalenga Zaidi kuwapatia vijana elimu ya usafi ili waweze kufahamu njia mbalimbali za kuepuka na kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Wakati huo Taasisi ya Raleigh Tanzania leo imefanya usafi katika soko la Chang’ombe na kukakabidhi mafangio 10, vifaa vikubwa vitano vya kuhifadhia taka, reki za kuvutia uchafu 3, sabuni za kunawia mikono 3 na vitabu 18 vinavyoelezea usafi na kuhitimisha katika shule ya Sekondari Dodoma kwa kufanya tamasha la usafi na wanafunzi.