Nkonko wakomesha mimba shuleni, kwa kujenga bweni
9 April 2021, 8:37 am
Na; Seleman Kodima.
Uongozi wa Kijiji cha Nkonko kilichopo Wilayani Manyoni Mkoani Singida umefanikiwa kujenga bweni la wasichana katika Secondari ya Kijiji hicho ili kupunguza tatizo la mimba shuleni.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Nkonko Bw.Ezekiel Samwel ambapo amesema kutokana na tatizo la Mimba kwa wanafunzi kuendelea kuwepo kila mwaka Shuleni hapo ,uongozi wa Kata hiyo kupitia fedha za Jimbo umefanikiwa kukamilisha Ujenzi wa Bweni ambalo litakuwa Mwarobaini wa tatizo hilo.
Amesema baada ya kumalizika kwa likizo fupi ya wanafunzi ,wanampango wa kukutana na baadhi ya wazazi ili kushauriana namna gani ya kuwawezesha watoto wao kuanza kutumia Bweni hilo.
Aidha amesema uongozi wa Kata umebaini sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikisababisha mimba kwa wanafunzi ni pamoja na mazingira magumu hali ambayo inatoa ushawishi kwa wanafunzi wengi kujihusisha kimapenzi na vijana wa mtaani.
Diwani huyo amesema mpango wao wa muda mrefu ni kuhakikisha pia wanajenga bweni la wavulani ili kufanikisha lengo la wanafunzi wa jinsia zote kukaa shuleni hapo.
Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 wanafunzi wote waishi Shuleni ili kuepuka mazingira hatarishi mitaani.