Mchezo wa kriketi kuongeza mahudhurio ya wanafunzi
4 May 2023, 1:03 pm
Afisa michezo wilayani Kongwa amesema wanawajengea uwezo walimu waweze kuwasaidia watoto kumudu vitendo vya mchezo wa kriketi ili kupitia ubora wa timu za shule zao waweze kupata wachezaji wazuri wa kuunda timu za Wilaya na pia wapate fursa ya kuchaguliwa kujiunga na timu za Taifa za miaka 15, 17, 19 kwa upande wa wasichana na wavulana.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Walimu wahitimu wa mafunzo ya mchezo wa Kriketi wilayani Kongwa wamesema uwepo wa mchezo huo mashuleni unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya utoro mashuleni kwani watoto wengi wanavutiwa kucheza na kushiriki tangu ulipoletwa wilayani humo mwaka 2021.
Walimu hao wameeleza hayo wakati wa kufunga mafunzo ya Kriketi kwa walimu wa shule 12 za msingi na sekondari za kata ya Kongwa yaliyofanyika katika kituo cha shule ya msingi Viganga ambapo wameshukuru pia chama Cha Kriketi Taifa (TCA) kwa kuleta mafunzo hayo.
Kwa upande wake mratibu wa Kriketi wilaya Kongwa Bwana Khassim Nassoro amewasihi walimu hao kuyashika yote waliyofundishwa kwa vitendo na kwenda kuwapatia ujuzi huo wanafunzi mashuleni ili kuzalisha wachezaji mahiri wa Kitaita na kimataifa wa mchezo huo.
Aidha Kwa upande wake Afisa michezo wilaya Kongwa Bwana Kelvin Msumule amesema baada ya mafunzo hayo wanatarajia kufanya mafunzo kama haya katika kituo cha shule ya Pandambili.