Rais afanya mabadiliko baraza la mawaziri
31 March 2021, 2:02 pm
Na; Mariam kasawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri .
Rais Suluhu amefanya mabadiliko hayo leo Machi 31,2021 Ikulu Chamwino Dodoma wakati wa hafla ndogo ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango ambapo katika mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri rais amemteua katibu kiongozi mpya.
Katika uteuzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi wa Tanzania nchini Japan, Hussein Yahya Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi akichukua nafasi ya Dk. Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge.
Kwa upande wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Rais Samia Suluhu Hassan amemhamisha aliyekuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu kwenda Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Selemani Jafo amepelekwa kushika nafasi ya Ummy Mwalimu.
Mwigulu Nchemba amepelekwa wizara ya Fedha na Mipango akisaidiwa na Hamad Masauni na nafasi yake katika Wizara ya Katiba na Sheria imechukuliwa na aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Paramagamba Kabudi akisaidiwa na Jofrey Mizengo Pinda.
Balozi Liberata Mulamula ameteuliwa kuwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku Naibu wake akiteuliwa kuwa Mbarouk Nassoro Mbarouk.
Kwa upande wa Wizara ya Nchi ofisi ya Rais, utumishi na Utawala bora, ameteuliwa Mohamed Omary Mchengelwa,na Manaibu wake wakiwa ni Mwita Waitara pamoja na Deogratius Ndejembi huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Capt. George Mkuchika akipangiwa kazi nyingine
Wizara ya Uwekezaji imerejeshwa katika ofisi ya Waziri Mkuu na kutolewa ofisi ya Rais, huku Godrey Mwambe akiteuliwa kuwa Waziri wa wizara hiyo na Prof. Kitila Mkumbo akipelekwa wizara ya Viwanda na Biashara na Naibu wake akibaki yule yule Mhe. Exaud Kigahe
Pauline Gekul ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa wizara ya Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo, huku aliyekuwa naibu waziri wa wizara hiyo, Abdallah Ulega akipelekwa wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa naibu waziri.
Naye, Mwanaidi Ally Hamis ameteuliwa kuwa naibu waziri wa pili katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.