Vijana 300 kudahiliwa na Chuo cha Veta Bahi Julai 2023
4 April 2023, 1:03 pm
Amewapongeza wasimamizi wa ujenzi wa chuo hicho kwa kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopelekea chuo hicho kutokukamilika kwa wakati.
Na Benard Magawa.
Vijana wapoatao 300 wanatarajiwa kuanza kunufaika na elimu ya ufundi stadi veta mara tu chuo cha Veta Bahi kitakapokamilika na kufunguliwa rasmi Julai 2023.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo cha Veta Dodoma Stanslaus Ntibala wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo hicho kwa Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi wilayani Bahi ilipofika kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho.
Amesema kwa kuanza chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wapatao 300 katika fani sita ambazo zitaanza kutolewa chuoni hapo ambazo ni uhazili na komputa, ushonaji, uashi,umeme wa majumbani,ufundi magari, na uchomeleaji vyuma.
Pia chuo kinatarajia kutoa mafunzo ya muda mfupi yatakayotokana na fani hizo.
Chuo hicho ambacho hadi sasa kimegharimu zaidi ya shilingi Billioni 2.2 kinatarajiwa kuwaongezea maarifa vijana wa Bahi na Tanzania kwaujumla ili wawe na uwezo wa kujiajiri wenyewe katika fani mbalimbali bila kusubiri kuajiriwa.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bahi Stuwart Masima akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa chuo hicho amesema wananchi wa wilaya ya Bahi na viongozi wapo tayari kutoa ushirikiano kwa uongozi wa veta katika kuhakikisha vijana wao wanaanza kukitumia chuo hichona kujipatia maarifa mbalimbali.
Aidha amewapongeza wasimamizi wa ujenzi wa chuo hicho kwa kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopelekea chuo hicho kutokukamilika kwa wakati kwani ni muda mrefu tangu kilipoanza kujengwa.