JKT yatarajia kuadhimisha miaka 60 ya kuasisiwa kwake
3 March 2023, 10:42 am
Madhimisho hayo ya miaka 60 ya kuasisi kwa Jeshi la Kujenga Taifa Jkt Tanzania yatafanyika uwanja wa jamhuri jijini Dodoma ambapo yamebeba kauli mbiu isemayo Malezi ya Vijana ,uzalishaji mali na Ulinzi kwa ustawi wa Taifa.
Na Seleman Kodima
Jeshi la kujenga Taifa JKT linatarajia kuadhimisha miaka 60 ya kuasisiwa kwake kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu,kufanya usafi wa mazingira katika maeneo hospitali ,upandaji wa miti na utoaji wa msaada kwa kwa wahitaji .
Pia wanatarajia kufanya mashindano ya mbio za riadha ,na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na SUMA JKT,vikosi,vyuo vya ufundi stadi na shule za sekondari .
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa MEJA JENERALI Rajabu Mabele wakati akizungumza na wahariri wa Vyombo vya habari na waandishi wa habari Makao makuu ya Jeshi la kujenga Taifa Chamwino Mkoani Dodoma .
MEJA JENERALI Mabele amesema July 10 mwaka huu JKT imepanga kufanya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuasisi kwa jeshi hilo Mwaka 1963 ambapo amesema mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu Dkt Samia Suluhu Hassan .
Amesema pamoja na Jeshi la kujenga Taifa kuwa na Majukumu yake ya msingi ya malezi ya Vijana ,uzalishaji mali na ulinzi pia wamekuwa wakifanya maboresho mbalimbali ili kuendana na wakati pamoja na mabadiliko ya sanyansi na teknolojia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho ya miaka 60 ya JKT kanali George Kazaula amesema kuwa maadhimisho hayo wanatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za serikali,binafsi na taasisi za kifedha .