Kukamilika kwa daraja la kiselu kutasaidi kukuza uchumi wa Sunya, Gairo na Kongwa
18 August 2021, 1:46 pm
Na; Selemani Kodima.
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la kiselu wilayani kiteto kunatajwa kusaidia kuchochea uchumi wa wakazi wa kata ya Sunya pamoja na wafanyabiashara wa maeneo ya Gairo na Kongwa.
Akizungumza na Dodoma FM Diwani wa kata ya Sunya wilayani Kiteto Bw. Mussa Brytoni amesema changamoto ya miundombinu hususani barabara inayounganisha kata ya Sunya imesababisha hali ya kibiashara pamoja na shughuli za kijamii kuwa mbaya msimu wa masika.
Amesema utatuzi wa miundombinu hiyo ikiwemo daraja la kiselu tayari imetegewa bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22 hivyo ni muda wa kusubiri utekelezaji wa Tanroads.
Aidha Diwani huyo amesema ubovu wa miundombinu umechangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha maendeleo ya jamii pamoja na wafanyabiashara wa Wilaya ya Kiteto, Sunya, Gairo na Kongwa.
Pamoja na hayo changamoto ya miundombinu hususani daraja la Kiselu linalounganisha kata ya sunya limekuwa kikwazo hasa katika msimu wa mvua katika upatikanaji wa huduma za msingi ikiwemo Elimu na Afya.