Serikali kuanza ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini
24 January 2024, 9:29 pm
Kampeni hiyo inatekelezwa katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, ambapo viongozi wa mikoa husika watashirikiana na UCSAF katika utekelezaji..
Na Mariam Kasawa.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauyeleo tarehe 24 Januari, 2024 amezindua Kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 unaotelekezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF).
Akizindua Kampeni yenye lengo la kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa mradi huo Mh. Nape amewataka viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma kuwa mabalozi wazuri wa Serikali kwa kuisemea vema kwa wananchi.
Amesema moja kati ya hatua muhimu iliyofikiwa hadi sasa ni pamoja na kutolewa kwa vibali vyote vya ujenzi wa minara 758. Hatua hiyo imewezesha kuanza kwa ujenzi wa minara katika maeneo ya utekelezaji wa mradi.
Aidha ameongeza kuwa, hadi kufikia tarehe 24 Januari, 2024 jumla ya minara tisa( 9) imejengwa na kukamilika, na tayari imewashwa, Jumla ya minara mingine 85 inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Bi Justina Mashiba ambao ni watekelezaji wa ujenzi wa minara hiyo ameelezea kuwa miradi hiyo ikikamilika watakuwa wamejenga minara 2146 ambayo itawaunganisha watanzania milioni 23 katika huduma ya mawasiliano.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amesema kuwa ujenzi wa minara hiyo unakwenda kutatua changamoto za mawasiliano vijijini ikiwemo Mkoa wa Dodoma na kuwa kichochea cha Maendeleo.
Dodoma Tv imezungumza na baadhi ya wananchi jijini hapa na kuwauliza je ujenzi wa Minara katika maeneo ya vijijini utasaidi kwa kiasi katika maendeleo?
Mnamo tarehe 13 Mei, 2023 Serikali iliingia makubaliano ya kuiongezea nguvu( upgrade) jumla ya minara 304 iliyokuwa inatoa huduma kwa Teknolojia ya 2G pekee Hadi sasa minara 190 kati ya hiyo ineongezewa nguvu ambapo inatoa huduma kwa teknolojia ya 3G na 4G.( sauti na data/ intaneti).