Waziri Mkuu atoa Tamko mradi uboreshaji milki za Ardhi
28 November 2023, 6:00 pm
Mradi huu unatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano (5) na una vipengele vinne (4) ambavyo ni Kuongeza Usalama wa Milki; Kuimarisha Mifumo ya Taarifa za Ardhi; Kujenga Miundombinu ya Ardhi na Usimamizi wa Mradi.
Na Seleman Kodima.
Wakurugenzi wa Halmashaurii nchini wametakiwa kuhakikisha katika kipindi hiki cha maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2024/25 wanatenga fedha kwa ajili ya sekta ya ardhi ili kuendeleza utekelezaji wa mradi wa kuboresha usalama wa Miliki za Ardhi katika maeneo ambayo mradi huo haujafika.
Pia katika maeneo ambayo Mradi huo unatekelezwa Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Timu za Utekelezaji wa Mradi wa LTIP .
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mh. kassim majaliwa ambapo Waziri wa Ardhi Jerry Silaa alimwakilisha katika Mkutano wa kitaifa mkuu wa wadau wenye lengo la kujadili utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usalama wa Miliki za Ardhi _LITP uliofanyika katika ukumbi wa Mabele – Mabeyo Complex Jijini Dodoma .
Nae Katibu Mkuu wizara ya Ardhi Waziri wa Ardhi Jerry Silaa akitoa taarifa ya Mradi huo amesema moja ya changamoto inayoukabili mradi huo katika utekelezaji kwa sasa ni wanufaika wengi ambao maeneo yao tayari yameshafanyiwa urasimishaji kushindwa kupata hati zao kwa kukosa namba za NIDA ambazo ndizo zinazotambulika katika mfumo wa umilikishaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amepongeza mradi huo ambao unaenda kutatua changamoto zinazohusiana na masuala ya ardhi hasa kwa Mkoa wa Dodoma.
Januari 21 2022 Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilisaini makubaliano na Benki ya Dunia ya mkopo wa Shilingi bilioni 346 sawa na dola za kimarekani milioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usalama wa Miliki za Ardhi nchini.