Udhibiti sumukuvu kukuza mnyororo wa thamani katika biashara
9 June 2023, 8:38 am
Kupitia mafunzo hayo washiriki wameweza kufahamu maana ya sumukuvu na madhara yake kwa afya ya binadamu.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Wadau mbalimbali wa kilimo cha karanga na mahindi katika kata ya Mtanana wilayani Kongwa wamepatiwa mafunzo juu ya udhibiti wa sumukuvu katika mazao kwa lengo la kuimarisha usalama wa chakula, lishe na kukuza pato la mkulima mmojammoja na taifa kwa ujumla.
Wakiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku tatu yanayotekelezwa na shirika la viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ikiwa ni sehemu ya mradi wa kudhibiti sumukuvu nchini (TANIPAC) washiriki hao wamesema kuwa kupitia mafunzo hayo wameweza kufahamu maana ya sumukuvu na madhara yake kwa afya ya binadamu.
Kwa upande wake Afisa viwango mwandamizi kutoka shirika la viwango nchini Bi Lilian Gabriel amefafanua kuwa washiriki wamepatiwa elimu juu ya sumukuvu na jinsi ya kudhibiti kuanzia mazao yanapokuwa shambani hadi kuhifiadhiwa katika maghala.
Akifunga mafunzo hayo mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel ameongeza kuwa sumukuvu imekuwa ikiathiri sana uchumi wa wakulima na wafanyabiashara hivyo ni vyema ikidhibitiwa ili kukuza mnyororo wa thamani katika biashara.
Aidha Mwema amewaagiza viongozi wa vijiji walioshiriki mafunzo hayo kuhakikisha elimu hiyo inatolewa na kuwafikia wananchi katika kila mikutano ya bajeti suala hili liwekwe kwenye ajenda ili kuwasaidia wananchi kuepukana na madhara yatokanayo na kuvu.