Wadau wa lishe waombwa kuisaidia jamii kufahamu umuhimu wa lishe bora
1 June 2023, 1:17 pm
Jamii inapaswa kuzingatia ulaji wa mlo kamili unaojumuisha makundi yote ya vyakula vya jamii ya nafaka, ya mizizi, ya wanyama, ya mikunde mbogamboga matunda sukari na asali.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Wadau wa lishe nchini wameombwa kusaidiana na serikali kuisaidia jamii kupata lishe bora ili kuondokana na udumavu na utapiamlo.
Hayo yameelezwa na afisa lishe wilaya Kongwa Bi. Mary Haule katika taarifa yake ambapo amesema kuwa kwa takwimu za hivi karibuni zinaonesha hali ya lishe katika wilaya ya Kongwa kwa watoto chini ya miaka mitano kiwango cha udumavu kimefikia asilimia 30.2.
Bi. Haule amezitaja sababu zinazopelekea hali hiyo ya udumavu kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu lishe na wazazi kuegemea zaidi katika harakati za utafutaji mfano kilimo kuliko kuwazingatia watoto katika suala la ulaji na lishe bora.
Kwa upande wake Bi. Olipa Fumbi kutoka shirika la lisilokuwa la kiserikali la UFUNDIKO linalojihusisha na masuala ya lishe kwa watoto wenye umri kuanzia miezi sita amesema wametengeneza siagi na unga lishe wenye makundi yote ya vyakula na kuwapatia bure watoto wenye uhitaji ili kujenga jamii yenye afya bora.