Jitihada zaidi zahitajika kuteketeza taka za kieletroniki
7 November 2024, 5:55 pm
Na Mariam Kasawa.
Takribani tani 33, 000 za taka za kieletroniki huzalishwa nchini kwa mwaka na asilimia 3% tu ya taka hizo hukusanywa na kurejereshwa na kiwango kikubwa cha taka hubaki na kuzagaa katika mazingira.
Bi Lilian Lukambuzi Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa mazingira na Jamii kutoka Baraza la usimamizi na uhifadhi wa mazingira NEMC anasema taka hizi zinakusanywa kwa kiasi kidogo na nyingi kubaki katika mazingira hivyo jamii inapaswa kuona fursa dhidi ya taka hizi.
Ripoti ya taarifa kwa umma kuhusu kanuni za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi za mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, imebainisha kuwa ongezeko la taka za kielektroniki linachochewa na kuongezeko kwa matumizi ya bidhaa za kielektroniki hasa simu, kompyuta, runinga na redio.
Bi. Lilian anaeleza moja ya changamoto iliyoibuliwa katika sera mpya ya mazingira ya mwaka 2021 ni pamoja na udhibiti wa taka za kielekroniki.
Kwa mujibu wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), kila mwaka tani milioni 50 za taka za kielektroniki huzalishwa duniani zikiwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 62 sawa na Sh142.4 trilioni.
Ripoti ya Taifa ya masuala taka za kielektroniki Tanzania Bara ya mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa, mwaka 2007, Tanzania ilizalisha jumla ya taka za kielektroniki tani 12,500 Miaka 10 baadaye taka hizo ziliongezeka mara mbili zaidi ya zilizokuwepo mwaka 2007 Ripoti hiyo inaeleza hadi kufikia 2017, uzalishaji wa taka hizo uliongezeka kwa asilimia 65 .