Jamii yatakiwa kupinga ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike ili kumuandaa mama bora wa badae
27 August 2021, 12:54 pm
Na; Benard Filbert.
Jamii inakumbushwa kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto wakike hali itakayosaidia kumuandaa mama mwenye malezi bora kwa familia yake hapo baadae.
Hayo yameelezwa na Bi. Stellah Matelu kutoka shirika lisilo la kiserikali la Action For Community Care ACC ambalo linajihusisha na haki za binadamu wakati akizungumza na Dodoma fm.
Amesema ukatili wa kijinsia umekuwa ukipingwa katika makundi mengi na sio vyema kulalamikia mapungufu ya mwanamke akiwa mkubwa bali anatakiwa kuandaliwa angali bado mdogo.
Kadhalika amesema changamoto kubwa inayopelekea ukatili wa kijinsia ni ndoa za utotoni ambapo katika Mikoa mitatu ambayo ina vitendo hivyo ni pamoja na Mkoa wa Dodoma huku elimu ikihitajika kwa kiwango kikubwa.
Issa Mohamed ni afisa uhamasishaji kutoka shirika la Restless Development ambalo linajihusisha na elimu ya makuzi kwa vijana Nchini amesema kuna sababu nyingi ambazo zimekuwa zikichangia ukatili wa kijinsia ikiwemo umasikini katika jamii.
Shirika la Action For community Care limekuwa likihudumu katika jamii kwa Nyanja mbalimbali ikiwemo kulinda na kutetea haki za binadamu.