Serikali yakiri kutoa Elimu bila Ada na sio Elimu bure
7 June 2021, 2:20 pm
Na; Yussuph Hans.
Serikali imesema inatoa Elimu bila Ada sio Elimu bure hivyo Wazazi washiriki kutoa michango kwa ajili ya maendeleo ya Shule.
Hayo yamebainishwa hii leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mh.David Silinde alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani, aliyehoji licha ya serikali kutangaza Elimu bure bado kumekuwepo na uchangishwaji wa Michango kwa Wazazi
Mh.Silinde amesema waraka wa Serikali namba 3 wa 2016 ulieleza ushirikishwaji wa Wazazi katika maendeleo ya Shule lakini Shule hairuhusiwi kufukuza Watoto kwa sababu ya michango
Ameongeza katika waraka huo umeainisha wajibu wa jamii, ambapo Wananchi wanatakiwa kushiriki katika Miradi ya Maendeleo ya kiserikali ikiwemo kujenga miundombinu ya shule.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako, amesisitiza kuwa ni marufuku mwanafunzi kufukuzwa shuleni kwa sababu ya michango huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu.
Dhana ya elimu bila ya ada ilikuwa ni miongoni mwa vipaumbele vinavyotekelezwa na Serikali tangu awamu ya tano hadi hii ya sita.