Changamoto ya zahanati chamwino wanawake kujifungulia njiani
21 May 2021, 1:27 pm
Na; Benard Filbert
Ukosefu wa huduma ya Zahanati katika Kijiji cha Chitabuli Wilayani Chamwino imetajwa kuwa changamoto kwa wananchi hivyo kusababisha wajawazito kujifungulia njiani.
Hayo yameelezwa na baadhi ya wakazi wa Kijiji hicho wakati wakizungumza na taswira ya habari kuhusu upatikanaji wa huduma za afya.
Wamesema kuwa Kijiji hicho hakijawahi kuwa na Zahanati hali inayowalazimu kutembea kilomita zaidi ya tano hadi Kijiji jirani kutafuta huduma za afya.
Keneth Msinzwa ni mwenyekiti wa Kijiji cha Chitabuli ameiambia taswira ya habari kuwa Kijiji hicho bado ni kipya hivyo wameanza kuchangisha wananchi michango itakayosaidia kuanza ujenzi wa Zahanati.
Naye diwani wa Kata ya Membe Simon Macheo amesema hivi sasa wamewekeza nguvu katika kuchangisha wananchi na zoezi la ujenzi wa Zahanati huenda likaanza mwaka huu.
Ukosefu wa zahanati katika maeneo ya vijijini imekuwa changamoto kubwa hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma za afya na wengine kulazimika kutembea umbali mrefu.