Wanafunzi watakao faulu kununuliwa mahitaji yote ya msingi Kongwa
14 March 2023, 1:14 pm
Halmashauri ya wilaya ya Kongwa kujipanga kuwanunulia mahitaji yote ya msingi wanafunzi wenye wazazi wasiojiweza kiuchumi watakaofaulu.
Na Alfred Bulahya.
Halmashauri ya wilaya ya Kongwa imepanga kuanza kuwanunulia mahitaji yote ya msingi wanafunzi wenye wazazi wasiojiweza kiuchumi watakaofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila, wakati akizungumza na wadau wa Elimu katika kikao cha mwaka cha wadau, kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kongwa.
Aidha amesema wanafunzi watakaofaulu kwa daraja la kwanza na kukosa nafasi kwenye shule za bweni, Halmashauri imetenga bajeti kuziwezesha shule mbili za bweni za Zoissa na Sejeli kuwapokea kama motisha kwa kufanya vizuri mitihani yao.
Akiwasilisha taarifa ya tathmini ya hali ya ufaulu kwa shule za msingi na sekondari, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa Bi. Margareth Temu amesema upungufu wa walimu, ukosefu wa chakula shuleni, na mwamko duni wa jamii, ni changamoto zinazorudisha nyuma ufaulu wa wanafunzi.
Mgeni Rasmi Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa amewataka viongozi kusimamia kikamilifu miradi yote inayoendelea na inapotokea changamoto watoe taarifa kwa ajili ya ufuatiliaji.
Katika Hafla hiyo Mgeni Rasmi alikabidhi zawadi mbalimbali zilizoandaliwa na Halmashauri kwa wanafunzi, walimu na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa mwaka 2022.