Wakazi wa Igungulile walazimika kutumia maji ya Mabwawa
21 January 2023, 10:13 am
Na; Victor Chigwada.
Kukosekana kwa huduma ya Maji safi na salama imetajwa kuwa ni sababu ya Wananchi wa kijiji cha Igungulile wilayani Chamwino kutumia maji ya mabwawa.
Mwenyekiti wa kijiji cha Igungulile Bw.Hamisi Msangi amesema changamoto ya maji imesababisha wananchi wake kutumia maji ambayo sio safi na salama.
Msangi amesema kuwa licha ya juhudi za serikali kuchimba visima virefu lakini maji hayo yamekuwa na wingi wa chumvi hali ambayo hayafai kutumiwa na binadamu.
Mwenyekiti huyo amesema njia mbadala itakayowezesha kutatua tatizo hilo ni serikali kuwasaidia kuunganisha mtandao wa bomba za maji kutoka kijiji jirani ili kuondokana na adha ya kutumia maji ya mabwawani
Naye Diwani wa Kata ya loje Wilaya ya Chamwino Bw.John Njohoka amekiri licha ya chngamoto hiyo lakini wanaishukuru Serikali kwa msaada wa baadhi ya visima
Amesema baadhi ya visima vimegundulika kuwa na maji yenye chumvi kali ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu na kuiomba Serikali kuendelea na jitihada za kupeleka huduma.