Waziri wa maji akutana na uongozi wa Benki ya Exim kutoka India
3 November 2021, 1:21 pm
Na; Mindi Joseph.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amekutana na uongozi wa Benki ya Exim India kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28 ambao ni moja ya miradi ya maji iliyopangwa kutekelezwa na Serikali.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Maji, Mji wa Serikali Jijini Dodoma kwa lengo la kukamilisha taratibu muhimu na kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.
Waziri Aweso ameushukuru uongozi wa Benki ya Exim India kwa kusafiri kuja nchini mahsusi kwa kukutana na Serikali ili kuona utekelezaji wa mradi huo unaanza, na kusema mpango wa Serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi inafika asilimia 95 katika maeneo ya mijini na asilimia 85 vijijini.
Waziri amewataka Benki ya Exim kuhakikisha wanatoa kibali haraka ili mikataba ya ujenzi wa mradi wa miji 28 inasainiwa kwa sababu kibali hicho kimechelewa kutolewa kwa muda mrefu.
Amesema India ni moja ya washirika wakubwa wa Sekta ya Maji na kielelezo ni mradi mkubwa wa maji wa Tabora-Igunga-Nzega uliokamilika kwa kiasi cha shilingi bilioni 600, na wananchi zaidi ya milioni 1.2 wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.
Mhe. Aweso ameainisha kuwa Wizara ya Maji sio kikwazo katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma ya maji, na lengo la Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani katika kona zote za nchi.
Akiongea katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema wanufaika wa mradi huo wanasubiri kuona kazi inaanza na viongozi wamejipanga kuratibu kazi mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema japo mradi huo umechukua muda kuanza kupitia vikao hivi vinavyofanyika hivi sasa matarajio ya kuanza kwa mradi huo ni makubwa.
Ujumbe wa Benki ya Exim India umeongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bw. Gaurav Bhandari aliyesema uhusiano kati ya India na Tanzania ni mkubwa na wa siku nyingi, na kuahidi kampuni bora zitatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini. Mradi wa maji wa miji 28 umepangiwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 ikiwa ni zaidi ya shilingi trilioni moja ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India.