Chanjo ya UVIKO 19 inamuepusha mtu alie chanjwa dhidi ya homa kali na madhara yake pindi akiambukizwa virusi vya korona
2 September 2021, 1:42 pm
Na;Yussuph Hans.
Inaelezwa kuwa moja ya sababu kubwa ya kupata chanjo ya UVIKO-19 ni kumuepusha mtu aliyechanjwa dhidi ya homa kali, pamoja na madhara yake pindi akiambukizwa virusi vya Korona.
Hayo yamebainishwa na Mtaalamu kutoka kikosi kazi cha kitaifa cha kutoa elimu ya chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi Dkt Elichiua Shao, wakati akizungumza na kituo hiki juu ya umuhimu wa kinga ya UVIKO-19 Mwilini.
Amesema kuwa chanjo imepitia hatua mbalimbali uchunguzi na hatimae kuthibitishwa kuwa inafaa kutumika hivyo watanzania hawapaswi kuwa na hofu juu ya chanjo hiyo kwani ni salama na haina madhara.
Ameongeza kuwa suala la maudhi madogo madogo ni ya kawaida katika matumizi ya dawa mbalimbali ikiwemo chanjo.
Taswira ya Habari imezungumza na baadhi ya wakazi katika Jiji la Dodoma ambapo wamesema bado jamii imekuwa na ugumu katika kupata chanjo ya UVIKO-19 huku baadhi yao waliofanikiwa kupata chanjo hiyo wakikiri kupata maudhi ya kawaida.
Tanzania bado inaendelea na zoezi la utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 katika vituo mbalimbali vya afya ili kukabiliana na Janga la Korona.