Mgogoro wa ardhi wakwamisha ujenzi wa vyoo vya gulio Chilonwa
24 August 2021, 2:02 pm
Na; Selemani Kodima.
Imeelezwa kuwa mgogoro wa eneo ambalo lilitakiwa kujengwa matundu ya vyoo katika Gulio la Chilonwa ni sababu ya kuchelewa ujenzi wa matundu hayo.
Hayo yameelezwa na Diwani wa Kata ya Chilonwa Bw Alpha Msuza wakati akielezea mkakati unaoendelea kufanyika kutatua changamoto ya Ukosefu wa Vyoo bora katika Gulio la Chilonwa wilayani Chamwino.
Amesema sababu inayokwamisha ujenzi wa vyoo katika Gulio hilo ni mgogoro wa ardhi uliyoibuka baina ya wananchi wawili kudai eneo ambalo linatarajiwa kujengwa vyoo hivyo ni eneo lao.
Bw Msuza amesema hatua waliochukua ni kuwaandikia barua wananchi hao na wanategemea kuwafikisha katika baraza la usuluhishi wa migogoro ndani ya kata ya chilonwa
Aidha Diwani huyo amewataka wananchi kuwa na utambuzi juu ya Maeneo ambayo ni maalumu kwa ajili ya utoaji huduma za kijamii na kuacha mtindo wa kukwamisha maendeleo ya serikali.
Pamoja na hayo amewataka wananchi kuwa pamoja katika utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa vyoo bora hali itakayosaidia upatikanaji wa huduma hiyo.