Wakazi Mkoani Dodoma waomba kuboreshewa huduma kupitia mfuko wa jamii wa CHF
11 August 2021, 12:48 pm
Na;Yussuph Hans.
Wakazi mkoani hapa wameomba kuboreshewa huduma zinazopatikana kupitia mfuko wa afya wa jamii (CHF) hususani maeneo ya vijijini ikiwemo vipimo pamoja na upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya.
Wakizungumza na kituo hiki baadhi ya wakazi hao wamesema kuwa bima hizo zinawasaidia kwa kiasi kikubwa, lakini changamoto ni uhaba wa dawa pamoja na vipimo.
Wamoengeza kuwa licha ya gharama ya bima hiyo kuwa nafuu na kuzidi kuboreshwa kuna umuhimu wa serikali kuongeza idadu ya vituo vya kutolea huduma pamoja na idadi ya vipimo.
Hivi karibuni mratibu wa CHF MKOA dokta Francis Rutalala Akizungumza na waganga wafawidhi kutoka zahanati mbalimbali mkoani hapa juu ya uhamasishaji na utoaji Elimu ya Mfuko wa Afya wa Jamii amesema kuwa maelekezo ambayo yametolewa na mkoa ni kufikia asilimia 30 hivyo waganga wafawidhi wanajukumu la kutoa hamasa mara kwa mara kwenye vituo vyao vya Afya ili kuhakikisha wananchi wanapata kadi za CHF.
Mfuko wa Afya ya Jamii Ni mpango muhimu wa hiari ulioanzishwa kwa Sheria Na. 1 ya mwaka 2001 (Sura ya 409 ya Sheria za Tanzania Toleo la 2002) wa kaya, kikundi au familia au mtu binafsi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua, Mwanachama atanufaika na huduma zote za afya ya msingi za kinga na tiba zitolewazo katika zahanati, kituo cha afya na hospitali ya wilaya.