Wakulima wa zao la Mtama mkoani Dodoma wanufaika na masoko ya uhakika
26 July 2021, 8:47 am
MAKALA
Na;Mhindi Joseph.
Mtama ni miongoni mwa mazao ya nafaka yanayolimwa kwa wingi nchini na duniani kote. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula na biashara na lina stahimili hali ya ukame likilinganishwa na mazao mengine ya nafaka.
Kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi zao la mtama limegeuka lulu katika maeneo mbalimbali hapa nchini na miongoni mwake ni Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Tanzania inatajwa kuwa nchi bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, kwa kuzalisha mtama bora, hivyo ni vema wakulima wakatumia mwanya huo kukuza uchumi wao kwa kuzalisha kwa tija ambapo kwa sasa mradi wa shirika la Mpango wa Chakula duniani (WFP) wa kilimo himilivu cha zao la mtama (Climate Smart Agriculture Project) unao fadhiliwa na Ubolozi wa Ireland hapa Tanzania (Irish Embassy in Tanzania) na kutekelezwa na shirika la Farm Africa umewezesha wakulima kulima kwa tija na kibiashara na kwa sasa uzalishaji umeongeza kutoka Kilogramu 300 na kufikia Kilogramu 750 kwa ekari na bei ya kongeza kutoka shilingi za kitanzania 250/= mpaka kufikia 550/= kwa kilo moja ya Mtama. Mradi unaendelea kuwajengea uwezo wakulima wa mtama ili kufikia lengo la kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la Mtama kutoka Kilogramu 750 mpaka 1,000 kwa ekari kwa msimu wa uzalishaji 2021/2022.
Katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchini wakulima wa Mkoani Dodoma wameshauriwa kuendelea kulima mazao yanayostahimili ukame ikiwemo zao la Mtama.
Mwandishi wa makala hii amehudhuria mdahalo ulioandaliwa na shirika la Farm Africa shirika linalolenga kukuza zao la mtama kwa Wakulima na kuongeza uzalishaji wa chakula wenye ufanisi.
Na katika wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma katika kijiji cha Chamae kata ya Hogoro wakulima wameanza kunufaika na zao la mtama kupitia kupata masoko ya uhakika ambapo mpaka sasa tani 125 zimeuzwa na wakulima 84 kupitia kampuni ya TBL na wakulima kuingiza kipato ghafi cha jumla shilingi 68,750,000/=.
Kedimoni Yohana Masikini ni mkazi wa Chamae na mwanakikundi wa kikundi cha Tumaini Mtama, ameomba Serikali na washirika wa maendeleo kuendelea kuboresha upatikanaji zaidi wa mbegu bora za Mtama ili kuwa uzalishaji wenye tija zaidi kwa msimu ujao wa 2021/2022.
“Nilipata hamasa ya kulima mtama baada ya kubaini kuwa ni zao linaloweza kuwa mkombozi wangu katika chakula na biashara ambapo mwaka huu nifanikiwa kuvuna gunia 16 ndani ya ekari mbili (2) na nikauza kwa shilingi 550/= kwa kilo ambapo nilipata shilingi 880,000/= na kufanikiwa kununua ng’ombe wawili anasema Kedimoni Yohana”
Naye Judith Samweli mkulima na mwenyekiti wa kikundi cha Tumaini Mtama katika kijiji cha Chamae amelishukuru shirika la Farm Africa kwa kuandaa mdahalo huo ambao utaendelea kuwasaidia wakulima kuendeleza kilimo cha za Zao la mtama ambacho kinawasaidia zaidi kujikwamua kiuchumi kwa kuwa na uhakika wa chakula na kipato.
“Kwa kweli mtama ndiyo mkombozi wangu kwenye kilimo kwani umenisaidia kuwa na uhakika wa kulipia watoto wangu ada za shule kutokana na uzalishaji kuwa juu kwa sasa kwani tunauza kilo kwa shilingi 550 tofauti na awali tulikuwa tunauza shilingi 200 hadi 300 anasema Judith Samweli ”
Chochote kizuri hakikosi changamoto na vivyo hivyo kwa wakulima wa mtama ambapo mkulima Kedimoni Yohana na Judith Samweli wanazibainisha changamoto hizo kuwa ni kucheleweshwa kwa malipo yao kutoka kwa wakala wa kampuni ya TBL, ambapo msemaji wa Kampuni aliwaomba radhi wakulima kwa kuwa kampuni yao inaandaa mfumo bora wa kulipa wakulima unaoitwa Bank Q ambao utatumika kama mwarobaini wa kuondoa kero za ucheleweshwaji wa malipo ya wakulima.
Meshack Panga ni Afisa Mradi wa kilimo himilivu cha zao la Mtama kutoka shirika la Farm Africa Mradi katika wilaya ya Kongwa, anasema mpaka sasa wanufainka katika mradi huo ni wakulima 4,099 kati yao asilimia 51 ni wanawake na 49 ni wanaume. Ameongeza kuwa mradi unafanya kazi na vikundi vitano vyenye jumla ya wakulima 250 katika kijiji cha Chamae kata ya Hogoro ambao wote wamenufaika na mradi hasa kupata masoko ya uhakika kutoka kwa wanunuzi wakubwa wa mtama kama kampuni ya bia ya Tanzania (TBL Co. Ldt). Meshack ameongeza kuwa, Kwa msimu huu wa uzalishaji wa mtama (2020/2021) kampuni ya TBL inategemea kununua jumla ya tani 10,000 za mtama kutoka kwa wakulima wa Mtama ndani ya Wilaya tatu mkoani Dodoma ambazo ni Kongwa, Mpwapwa na Chamwino ambapo mpaka sasa wameweza kununua tani zipatazo 2000. Kwa wilaya ya Kongwa
“Wakulima 628 wameingia kwenye kilimo cha mkataba rasmi na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambapo kampuni hiyo iliwawezesha kupatikana kwa mbegu bora za mtama kwa njia mkopo na kutegemea wakulima kuzilipa kipindi cha masoko ambapo TBL itakata gharama za mbegu kwanza na kumpa mkulima fedha zake zilizosalia.
Naye Afisa Msimamizi wa Manunuzi kutoka kampuni ya KFS (Mr. Maziwa Ally) ambaye ni wakala wa TBL ndani ya wilaya ya Kongwa, ameongelea mpango wa kilimo cha mkataba cha Mtama umeweza kuondoa changamoto za masoko katika vijiji zaidi ya 80 katika wilaya ya Kongwa.
“Tumeangalia uwiano wa kuhakikisha kila enao tunafika na kununua mtama na katika kijiji cha Chamae mwaka huu tumefanikiwa kukusanya tani 125 anasema Afisa Msimamizi wa Manunuzi huyo”
Nini kauli ya Serikali kuhusu mtama?
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Kilimo katika wilaya ya Kongwa, Amina Msangi ambaye ni mratibu wa mradi wa Kilimo Himilivu anasema changamoto ya kutokupata mbegu bora za mtama kwa wingi imechangia wanachi wengi kulima mbegu sisizo na tija japo kwa sasa tunashirikiana na Mradi wa Shirika la Mpango wa Chakula duniani (WFP) unaotekelezwa na Farm Africa kuwekeza zaidi katika kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa wingi ambapo kwa sasa mashamba manne ya mbegu bora za mtama daraja la kuazimiwa (QDS farms) yameanzishwa na yanategemewa kuzalisha zaidi ya tani 6 za mbegu bora zitakazotumika kwa msimu ujao wa kilimo.
“Ameongeza kuwa Jogorafia ya kongwa inaruhusu zaidi wakulima kulima zao la mtama, sisi kama serikali tutaendelea kushirikiana na wadau ili kuongeza tija zaidi kwa kuhahakisha wakulima wanapata mbegu bora, elimu ya ugani na masoko ya uhakika”.
Amina Msangi anawaasa wasambazaji wa mbegu wasiokuwa waaminifu wenye tabia ya kuchanganya mbegu waache tabia hiyo mara mmoja, kwa kuwa hali hiyo inawasababishia wakulima kupata hasara kubwa, na kusabishia wilaya na hata taifa kukosa mapato yatokano na zao hili la mtama.