Ukosefu wa madarasa kwa shule za msingi watajwa kuwa chanzo cha matokeo mabaya Mkoani Dodoma
20 July 2021, 11:57 am
Na; Shani Nicolous.
Ukosefu wa madarasa katika shule za msingi na sekondari wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma imetajwa kuwa chanzo cha matokeo mabaya kwa wanafunzi hivyo kusababisha Mkoa wa dodoma kushika nafasi ya tatu kutoka mwisho kitaifa.
Akizungumza na Dodoma fm katika kipindi cha Dodoma live leo hii Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Gifty Isaya Msuya amesema kuwa ufaulu katika shule za Wilaya hiyo hauridhishi hivyo na hii ni kutokana na baadhi ya shule kukosa madarasa ya kusomea na kukaa chini ya mti.
Amesema kuwa kama Wilaya wameadhimia kuhakikisha wanaboresha miundombinu katika sekta ya elimu kama kujenga madarasa , nyumba za walimu pamoja kusimamia upatikanaji wa lishe kwa wanafunzi shuleni.
Akizungumzia kuhusu suala la ukatili amesema kuwa ushirkiano kutoka kwa maafisa mbalimbali pamoja na viongozi wa serikali utasaidia kutokomeza ukatili katika jamii ambao umekuwa ni chanzo cha kukatisha ndoto za wanafunzi mbalimbali na hata kukwamisha shughuli za kimaendeleo .
Kuhusu suala la kuhakikisha akina mama wajasiriamali wanapata mikopo nafuu mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa usimamizi mkubwa na wa hali ya juu unaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha asilimia zilizotengwa kwaajili ya akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalumu zinawafikia kama ilivyo azimiwa.
Akigusia ujio wa mwenge katika wilaya ya Chamwino Tarehe ishirini na tisa mwezi huu Mh.Msuya ameeleza maeneo yatakayo pitiwa na mwenge huo pamoja na miradi itakayozinduliwa siku hiyo.
Ameendelea kuwaasa wakazi wa Wilaya hiyo kuchukua tahadhari juu ya virus vya corona kwakufuata maelekezo wanayopewa na namamlaka ya afya na serikali.