Wakazi wa kata ya Iyumbu waishukuru serikali kwa kuwatatulia changamoto ya umeme
15 July 2021, 12:05 pm
Na; Victor Chigwada.
Wananchi katika Kata ya Iyumbu Jijini Dodoma wameishukuru Serikali kwa jitahada walizo zichukua katika kutatua changamoto ya umeme ndani ya Kata hiyo.
Wakizungumza na taswira ya habari baadhi ya wananchi hao wamesema wanayo furaha kuona muda si mrefu huduma ya nishati ya umeme ikiwafikia wananchi walio wengi kwani tayari kazi ya kufunga umeme inatarajia kuanza
Mwenyekiti wa mtaa wa Nyerere Bw. Ayubu Mandabaga amekiri kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme kwa baadhi ya mitaa lakini kwa sasa tayari zoezi la kusambaza nguzo na ufungaji wa nyaya za umeme litaanza muda wowote.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Bw. Eliasi Situchi amesema kuwa REA wapo tayari kuanza zoezi la ufungaji wa nyaya za umeme kwa taklibani nguzo tisini licha ya nguvu za TANESCO kusaidia kusambaza umeme kwa kipindi cha nyuma.
REA imekuwa na jukumu la kusambaza huduma ya umeme vijijini ili kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na upatikanaji wa nishati ya umeme Nchini