Dodoma FM

Taasisi na vyuo vya ufundi zimetakiwa kutoa elimu bora inayokidhi viwango.

28 May 2021, 1:21 pm

Na; MIND JOSEPH.

Serikali imezitaka taasisi pamoja na vyuo vinavyohusika kutoa elimu ya Ufundi nchini kuhakikisha vinatoa elimu bora inayokidhi viwango na mahitaji ya soko la ajira.

Hayo yamesemwa leo na waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa wakati akihutubia katika uzinduzi wa maonesho ya pili ya Elimu ya Mafunzo ufundi katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo amesema kuwa elimu ya ufundi ina umuhimu mkubwa kwa kuwa ndio kitovu cha mabadiliko.

Aidha Waziri Majaliwa amesema Serikali itaimarisha uhusiano wake na taasisi zinazotoa elimu ya ufundi nchini ,waajiri pamoja na sekta binafsi ili kuendelea kuzalisha rasimali watu itakayoweza kusaidia kufikia malengo ya serikali katika kukuza uchumi.

Awali wakati akimkaribisha Waziri mkuu, Waziri wa elimu sayansi na Teknolojia Mh. Joyce Ndalichako amesema kuwa lengo la maenesho hayo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa elimu ya ufundi nchini ili kujionea mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTE, Prof. John Kandoro amesema elimu ya ufundi inatilia mkazo katika mafunzo ya vitendo ili kufikia azma ya Serikali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na mafunzo ya elimu ya ufundi kwa fani mbalimbali yanayotolewa kwenye vyuo 430 Nchini.

Maonesho ya pili ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yamezindulia leo jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri na Waziri mkuu Mh.Kasimu Majaliwa ambapo maonesho hayo yameandaliwa na wizara ya elimu kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya ufundi pamoja na sekta binafsi na kauli mbiu katika maonesho hayo ni “KUIMARISHA USHIRIKIANO WA WADAU KATIKA KUKUZA UJUZI WA MAENDELEO YA UCHUMI WA VIWANDA”.