Wananchi wametakiwa kuunga mkono juhudi za kuhamasisha ubunifu wa teknolojia,
11 May 2021, 1:08 pm
Na; Fred Cheti .
Serikali imewataka wananchi kuunga mkono juhudi zake katika kuhamasisha ubunifu wa teknolojia ili matumizi yake yaweze kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa leo na waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa wakati akifunga maonesho ya kitaifa ya Sayansi , Teknolojia na ubunifu(MAKISATU) jijini Dodoma ambapo amesema kuwa serikali inatambua umuhimu mkubwa wa teknolojia hizo katika kukuza uchumi wa nchi na ni nyenzo muhimu katika kurahisisha maisha na kuokoa muda.
Aidha Mh.Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika ubunifu wa teknolojia ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na ujio wa mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo amesema kwa kuzingatia hilo serikali imeweka msukumo katika kujenga uwezo wa ndani wa sayansi, teknolojia na ubunifu ikiwemo kujenga mfumo imara wa Tehama kwa uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Job Ndugai ameiomba Serikali kuziangalia kwa ukaribu taasisi za utafiti na ubunifu ili ziweze kusogeza mbele uchumi wa nchi kulingana na matokea ya tafiti zao hasa katika maeneo ya kilimo, uchumi, na viwanda.
Leo ndio kilele cha Maonesho ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubinifu (MAKISATU) yaliondaliwa na Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia ambapo Maonesho hayo yalizinduliwa Mei 6 na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt.Joyce Ndalichako na Kufungwa leo na Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa na Kauli mbiu katika maonesho hayo ni “SAYANSI TEKNOLOJIA, NA UBUNIFU KWA UCHUMI ENDELEVU‘.