Wakazi wa kata ya Mpalanga walalamikia uchache wa miundombinu ya maji safi na salama.
10 May 2021, 10:27 am
Na; Victor Chigwada.
Changamoto ya upatikanaji wa maji imekuwa tatizo kubwa katika baadhi ya vijiji hali inayo pelekea wakazi wa maeneo hayo kutumia muda mwingi katika utafutaji wa maji.
Taswira ya habari ilitembelea Kata ya Mpalanga Wilaya ya Bahi katika vijiji vya Chidilo na Mpalanga ambapo wakazi wa maeneo hayo wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na miundombinu ambayo haikidhi mahitaji ya wananchi wa maeneo hayo.
Baadhi ya wanachi wa kijiji cha Mpalanga wakizungumza na taswira ya habari wamesema tatizo la uhaba wa maji katika maeneo hayo linatokana na uchache wa vituo vya kuchotea maji kwani baadhi ya mabomba yalipasuliwa wakati wa matengenezo ya barabara.
Bw. Marino Mgunda ni mwenyekiti wa kijiji cha Chidilo yeye amekili kuwepo kwa changamoto ya maji kijijini hapo, amesema wana visima viwili ambavyo havikidhi mahitaji huku mita za maji zilizofungwa katika vituo 14 nazo zikiwa na changamoto kwani hazifanyi kazi ipasavyo.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao Diwani wa Kata ya Mpalanga Bw.Baraka Ndahani amesema kuwa ni kweli mabomba yalikapasuka na kukatika kutokana na ujenzi wa barabara na tayari wapo kwenye matengenezo.
Hata hivyo Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jijini Dodoma DUWASA imekua na mkakati wa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.