Wagonjwa wa kifua kikuu watambuliwe mapema ili kuepusha maambukizi zaidi
14 January 2025, 2:49 pm
Kikao hicho maalum ni utekelezaji wa mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu katika halmashauri 76 za mikoa 9.
Na Seleman Kodima.
Katibu tawala mkoa wa Dodoma Kaspar Mmuya amesema ipo haja ya kuwatambua wagonjwa wa kifua kikuu mapema ili kuepusha kundi kubwa kuambukizwa maradhi hayo.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua kikao kazi cha kupanga namna bora harakishi na jumuishi ya kuwatafuta na kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu, kikao ambacho kimewajumuisha Waganga Wakuu wa Wilaya, Waratibu wa Kifua Kikuu na UKIMWI, Waratibu wa kifua kikuu na Ukoma pamoja na Wataalamu wa Maabara kutoka halmashauri 7 za Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Mmuya amesema ugonjwa wa kifua kikuu, usipoweza kumtambua mgonjwa mmoja, ana uwezo wa kuwaambukiza watu 15 hadi 20 kwa mwaka mmoja.
Aidha Mmuya amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, mwaka 2023 kulikuwa na wagonjwa Milioni 10. 8, kati ya hao Wagonjwa Milioni 1.25 walifariki dunia , ili hali Mwaka 2024 Tanzania ilikuwa na wagonjwa 122,000 ambapo wagonjwa 18,400 walifariki dunia .
Katibu Tawala huyo ameongeza kuwa ni muhimu kufahamu takwimu za ugonjwa, ili kuongeza jitihada za kukabiliana nao.
Kikao hicho maalum ni utekelezaji wa mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu katika halmashauri 76 za mikoa 9 uliozinduliwa Januari 06,2025 na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama katika kituo cha Afya Chamwino, kilichopo wilayani Chamwino wakati akikabidhi mashine za utambuzi na ugunduzi wa Ugonjwa wa kifua kikuu.