Jamii yaonywa kuacha kuwatumikisha watoto katika biashara.
4 May 2021, 9:02 am
Na; Thadey Tesha.
Katika kuondokana na wimbi la watoto wanaojihusisha na shughuli za biashara wakiwa na umri mdogo jamii imeshauriwa kuacha mara moja vitendo vya kuwatumikisha watoto wadogo katika shughuli za biashara kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Akizungumza katika mahojiano maalum na kipindi cha taswira ya habari afisa ustawi wa jamii wa jiji la Dodoma bi. Fauzia Mohammed amewashauri wazazi wanaowatumikisha watoto wao kujiingiza katika shughuli za biashara wakiwa na umri mdogo kuacha vitendo hivyo kwani ni miongoni mwa vitendo vya ukatili.
Aidha Bi Fauzia Mohammed amesema kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari amewataka waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na ustawi wa jamii ili kuendelea kutoa elimu zaidi katika jamii kutokana na vyombo hivyo kuwa karibu zaidi na jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi jijini hapa wamesema miongoni mwa sababu zinazowafanya wazazi wengi kuwafanyisha watoto wao biashara ni hali ngumu ya maisha huku baadhi yao wakisema vitendo hivyo ni kinyume na sheria.
Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ajira kwa watoto wadogo kwani zimekuwa zikiwaathiri watoto hao kisaikolojia pamoja na kimwili.