Keisha agawa mitungi 200 ya gesi kwa watu wenye ulemavu Dodoma
8 April 2024, 6:03 pm
Mbunge Keisha amemshukuru Rais Samia kwa kuwajali watanzania hususani watu wenye ulemavu nchini.
Miongoni mwa mkakati jumuishi wa serikali ni kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2033 zaidi ya 80% ya wananchi nchini wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na mkaa ulioboreshwa.
Katika kuunga mkono juhudi hizo Mbunge wa Viti Maalum Khadija Shabani Taya maarufu kama (Keisha) amempa tano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhimiza nishati safi ya kupikia ikiwa ni ajenda ya kumtua mama kuni kichwani ambapo amegawa mitungi 200 kwa watu wenye ulemavu Mmkoani Dodoma baada ya tukio la iftar iliyoandaliwa na mbunge huyo kwa watu wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine Mmgeni rasmi katika hafla hiyo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada mbalimbali katika kuwahudumia watu wenye ulemavu na wao kama Wizara wataendelea kufanya jitihada mbalimbali kuwazingatia watu wa kundi hilo.
Kwa Upande wake mwakilishi wa Mufti Shekh Harith Nkussa amewasisitiza watanzania na hususani waislamu kutoa mahitaji mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalum kama alivyofanya Mbunge Keisha.
Mbali na Viongozi hao wa Serikali ibada hiyo imehudhuriwa pia na Wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.