Mifugo ya mwenyekiti mstaafu yapewa sumu asema anaumuachia Mungu
8 November 2023, 5:21 pm
Ikumbukwe mtaa huo una mwenyekiti wa mtaa ambapo majukumu yake ni kusimamia na kuhamasisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao na wananchi wana haki na wajibu wa kulinda mali, rasilimali za umma na kupambana na kila aina ya uovu ikiwemo ubadhirifu, wizi ,rushwa na mengineyo kwa mujibu wa sheria
Na Victor Chigwada.
Wito umetolewa kwa wakazi wa mtaa wa Ihumwa A kuwa makini na watu wenye nia mbaya na wanaojihusisha na vitendo vya uharifu ambavyo vinahatarisha afya za wanajamii.
Hili linajiri baada ya hivi karibuni kuripotiwa taarifa ya mtu mmoja kusambaza kitu kinachodhaniwa sumu na kusababisha athari kwa mifugo kwa aliyewahi kuwa mwenyekiti wa mtaa huo.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa mtaa huo Bw.Wiliamu Njilimuyi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo na kukemea vitendo hivyo ambapo amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuwa mlinzi wa nyumba ya mwenzake.
Njilimuyi amesema kuwa kwa hivi karibuni watu wasiojulikana wamekuwa wakisambaza vitu vyenye sumu katika nyumba ya mwenyekiti mstaafu Bi.Victoria Joseph ambapo mpaka sasa mifugo kadhaa imekufa kutokana na vitendo hivyo.
Katika kufahamu undani wa mkasa huo, Taswira ya Habari imezungumza na Bi.Victoria Joseph mwenyekiti mstaafu wa mtaa huo ambapo amekiri kuandamwa na watu wanaodhaniwa kusambaza sumu katika nyumba yake huku wakimwaga sumu hiyo kwenye maandazi.
Bi.Victoria amesema vitendo hivyo vimekuwa vikimuumiza bila kujua nini anaweza kufanya na ameamua kumuachia Mungu juu ya changamoto hiyo.
Kwa upande wao baadhi ya majirani wa Bi.Victoria Joseph wamesema kuwa yaliyomkuta Mwenyekiti huyo Mstaafu yameleta athari kwa majirani wanaomzunguka kutokana na mifugo yao kufa kutokana na sumu iliyosambazwa na watu hao.