Teknolojia yatajwa kukwamisha usomaji wa vitabu
4 October 2021, 1:34 pm
Na; Thadei Tesha.
Mwitikio wa jamii juu ya usomaji wa vitabu umeendelea kuwa wa wastani kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kusoma vitabu hivyo ambapo kukua kwa teknolojia kukitajwa kuwa miongoni mwa visababishi.
Wakizungumza na taswira ya habari baadhi ya wananchi jijini hapa wamesema suala la usomaji wa vitabu limekuwa halizingatiwi kutokana na hamasa pamoja na gharama za vitabu kuwa juu huku teknolojia pamoja na ubize wa shughuli mbalimbali vikitajwa kama visababishi vikubwa.
Kwa upande wake mkutubi wa maktaba ya mkoa wa Dodoma Bi Judith Lugongo amesema mwitikio wa wananchi hususani jijini hapa umekuwa wa wastani ambapo ameitaka jamii katika makundi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kusoma vitabu mbalimbali katika maktaba hiyo ili waweze kunufaika na maarifa mbalimbali yaliyopo katika vitabu hivyo.
Aidha Bi Judith amewataka wazazi kuwajengea watoto wao utaratibu wa kwenda maktaba kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kusoma vitabu pamoja na kujifunza matumizi ya kompyuta kutokana na huduma hizo kutolewa katika maktaba mbalimbali zilizopo katika maeneo yao.
Usomaji wa vitabu ni moja ya njia ambazo zimekuwa zikitumika katika maeneo mbalimbali kama njia ya kuongeza maarifa katika jamii kutokana na mambo mengi kuandikwa katika vitabu hivyo.