Waziri Gwajima azindua rasmi baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNGO
10 July 2021, 2:19 pm
Na;Mindi Joseph .
Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt Doroth Gwajima amezindua rasmi baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNGO na kulitaka baraza hilo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo kwa kuzingatia sheria,kanuni na miongozo iliyopo ili kukidhi matarajio ya jamii na watazania.
Akizungumza mapema leo jijini Dodoma katika uzinduzi wa baraza hilo Dkt Gwajima amewapongeza viongozi wote 30 wa baraza waliochaguliwa na kuaminiwa na wajumbe katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania bara na makundi maalum.
Ameongeza kuwa viongozi hao waliochaguliwa wasiruhusu watu wachache kuirudisha NaCoNGO nyuma nakuligeuza baraza kuwa kitega uchumi na baada ya miaka mitatu anatarajia kuona uchaguzi unaitishwa tena pasipo kutegema waziri kuingilia kati mchakato wa sekta hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya mpito ya uchaguzi Wakili Flaviana Charles amelihimiza baraza lililochaguliwa kupitia kanuni hizo na kuzifanyia kazi ambazo zimekuwa za muda mrefu na zimepitwa na muda.
Naye Mwenyekiti mpya wa baraza la taifa la mashirika yasiyo yakiserikali NaCoNGO Lilian Joseph Badi ameahidi kuwa NaCoNGO mpya itajikita katika kazi,utendaji,uwajibikaji na kuimarisha mahusiano na wadau wengine pamoja na serikali.
Baraza la taifa la mashirika yasiyo yakiserikali NaCoNGO mara ya mwisho lilifanya uchaguzi wake mwaka 2016 na baada ya hapo uchaguzi haukufanyika tena baada ya viongozi waliokuwepo madarakani kumaliza muda wao na kukaidi kufanya uchaguzi mpaka waziri Gwajima alipoingilia kati na kuunda kamati ya wajumbe 10 na kutoa siku 30 uchaguzi huo kufanyika na umefanyika kwa Demokrasia haki na amani.