Mwenyekiti wa baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali atangaza mchakato wa uchaguzi kwa mikoa yote nchini
28 June 2021, 12:42 pm
Na;Mindi Joseph .
Mwenyekiti wa kamati wa baraza la taifa la mashirika yasiyo yakiserikali NaCoNGO Wakili Flaviana Charles ametangaza kuanza kwa mchakato wa uchaguzi katika ngazi ya mikoa yote nchini unaoshirikisha wawakilishi waliochaguliwa kutoka kila wilaya.
Akizungumza leo jijini Dodoma Wakili Flaviana Charles amesema uchaguzi huo utaanza leo June 28 hadi Julai 2 na utasimamiwa na viongozi walioteuliwa na kamati ya uchaguzi ya taifa na wasajili wasaidizi ngazi ya mikoa watakuwa waangalizi huru katika uchaguzi kwa mikoa husika.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia June 7 mwaka huu waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt Doroth Gwajima kufanya uteuzi wa kamati ya mpito kwa ajili ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa baraza la taifa la mashirika yasiyo yakiserikali ya kitaifa na kimataifa na kutoa muda wa siku 30.
Aidha wakili Flaviana amesema tathimini ya mwenendo wa uchaguzi wa baraza la taifa la mashirika yasiyo yakiserikali hususani katika ngazi ya wilaya uliofanyika June 26 ulifanyika kwa amani na utulivu katika wilaya zaidi ya 130 Tanzania bara.
Uchaguzi Mkuu wa Kitaifa wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini (NaCoNGO ) unatarajiwa kufanyika Julai 8,mwaka huu mkoani Dodoma na kabla ya Julai 10 Mwaka huu zoezi nzima la uchaguzi kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa linatakiwa kukamilika na viongozi wapya kukabidhiwa ofisi Rasimi.