TARURA wahakikisha ukarabati barabara Nzuguni Dodoma
26 May 2021, 1:24 pm
Na; Yussuph Hans
Wananchi wa Kata ya Nzunguni Jijini Dodoma wamehakikishiwa ukarabati wa Barabara za Kata hiyo kwa kiwango cha Lami kwa mwaka huu, kufuatia changamoto ya ubovu wa barabara inayowakabili kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijini(TARURA) Eng Goodluck Mbanga wakati akizungumza na Taswira ya habari kuhusu mkakati wao wa kumaliza changamoto ya Barabara Kata ya Nzunguni.
Eng Goodluck amesema kuwa wameshaanza usanifu wa Barabara hiyo ambayo itajengwa kwa kiwango cha Lami pamoja na Mifereji ili kudhibiti Maji yanatokana na Maeneo mbalimbali.
Ameongeza kuwa tofauti na changamoto ya Ardhi ya Nzuguni kuwa ya umaji umaji, changamoto nyengine ni kutokana na maeneo yake kurasimishwa ambapo upimaji ulichelewa pia imeshababisha Barabara zake kuwa nyembamba.
Sanjari na hayo Wakazi wa Nzunguni wameshauriwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambapo Serikali inaendelea na mkakati wa kukarabati barabara hiyo.
Ikumbukwe kuwa mara kadhaa Dodoma Fm imekuwa ikiripoti changamoto ya Barabara ya Nzuguni kwa Masista ambapo Barabara hiyo huharibika zaidi katika kipindi cha Msimu wa Mvua na kusababisha Adha ya usafiri pamoja na Nauli kupanda .