Barabara kata ya Mtanana A hadi Ndalibo kuanza marekebisho hivi karibuni
12 May 2021, 1:17 pm
Na; Benald Filbert
Barabara zilizopo katika kata ya Mtanana wilaya ya Kongwa zimeingizwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 ili kufanyiwa ukarabati kuanzia eneo la Mtanana A hadi Ndalibo, kwa lengo la kuondoa usumbufu ambao wananchi wamekuwa wakikutana nao.
Akizungumza na taswira ya habari diwani wa Kata ya Mtanana Joel Shadrack amesema Kata hiyo imekuwa na barabara korofi hali inayosababisha kukwama kwa baadhi ya shughuli za maendeleo.
Amesema kupitia bajeti ya Serikali barabara hizo zitafanyiwa marekebisho ambapo mwezi wa saba zitatangazwa zabuni kwa wakandarasi wenye vigezo vya kufanya kazi hiyo.
Amesema kukamilika kwa barabara hizo katika Kata ya Mtanana itafungua fursa mpya kwa wananchi kuongeza shughuli za ukuzaji wa uchumi.
Barabara nyingi zilikuwa zimeharibiwa na mvua hivyo serikali imekuwa ikijipanga kufanya marekebisho ili kuondoa usumbufu kwa wananchi ikiwepo kukwamisha shughuli za maendeleo.